Marko 5-10
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu
(Mt 8:28-34; Lk 8:26-39)
5 Wakafika ng'ambo ya ziwa, katika nchi walimoishi Wagerasi.[a] 2 Yesu alipotoka katika mashua ile ghafla, mtu mmoja aliyekuwa na roho chafu alitoka makaburini kuja kumlaki. 3 Mtu huyu aliishi makaburini, na hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga hata kwa mnyororo, 4 Watu walijaribu kila mara kumfunga kwa minyororo na vyuma kwenye miguu na mikono. Hata hivyo, aliweza kuivunja minyororo ile na pingu zile za vyuma wala hakuna aliyekuwa na nguvu za kutosha kumdhibiti. 5 Kila mara usiku na mchana akiwa makaburini na kwenye milima alipiga kelele na kujikata kwa mawe.
6 Alipomwona Yesu kutoka mbali, alimkimbilia, na kusujudu mbele yake. 7 Kisha akalia kwa sauti kubwa na kusema, “Unataka nini kwangu, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Mkuu zaidi? Nakuomba uape mbele za Mungu kwamba hutanitesa.” 8 Yule pepo alisema haya kwa sababu Yesu alikuwa anamwambia, “Mtoke huyo mtu, ewe pepo mchafu!”
9 Ndipo Yesu akamwuliza yule mtu, “Jina lako nani?”
Naye akamjibu, “Jina langu ni Jeshi,[b] kwa sababu tuko wengi.” 10 Yule pepo akamwomba Yesu tena na tena asiwaamuru kutoka katika eneo lile.
11 Kulikuwepo kundi kubwa la nguruwe likila katika kilima. 12 Wale pepo wakamwomba Yesu awatume waende katika lile kundi la nguruwe na kuliingia, 13 Naye akawaruhusu. Kwa hiyo pepo wachafu walimtoka mtu yule na kuwaingia nguruwe.[c] Kundi lile lilikuwa na idadi karibu ya elfu mbili, lilikimbia kuelekea kwenye kingo zenye mtelemko mkali na kutumbukia ziwani, ambamo walizama.
14 Wale waliowachunga walikimbia. Wakatoa taarifa mjini na katika maeneo jirani ya mashambani. Watu wakaja kuona ni kitu gani kilichotokea. 15 Watu hao wakamwendea Yesu. Nao wakamwona yule aliyekuwa na mashetani ameketi mahali pale, amevaa nguo na akiwa mwenye akili zake nzuri; huyu ni yule aliyekuwa amepagawa na jeshi la mashetani. Wakaogopa. 16 Wale waliokuwa wameona hili waliwasimulia kile kilichomtokea mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani na kuhusu nguruwe wale. 17 Nao wakamwomba Yesu aondoke katika eneo lile.
18 Wakati Yesu akipanda katika mtumbwi, mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani alimwomba Yesu afuatane naye. 19 Lakini Yesu hakumruhusu aende naye, isipokuwa alimwambia, “Nenda kwa watu wa kwenu, na uwaambie yote ambayo Bwana amekufanyia, na uwaambie jinsi alivyokuwa na huruma kwako.”
20 Hivyo mtu yule aliondoka, na akaanza kuwaeleza watu katika Dekapoli[d] mambo mengi ambayo Yesu amemtendea, na watu wote walistaajabu.
Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa
(Mt 9:18-26; Lk 8:40-56)
21 Kisha, Yesu alivuka kurudi upande wa magharibi wa ziwa. Pale kundi kubwa la watu lilikusanyika kwake. Yeye alikuwa kando ya ziwa, na 22 mmoja wa viongozi wa sinagogi, aliyeitwa Yairo, alifika pale. Naye alipomwona Yesu, alipiga magoti miguuni pake. 23 Kisha akamwomba kwa msisitizo, akisema, “Binti yangu mdogo yu karibu kufa. Ninakuomba ufike na kumwekea mikono, ili kwamba apone na kuishi.”
24 Hivyo Yesu alienda pamoja naye. Na kundi kubwa la watu lilimfuata; nao walikuwa wakimsonga pande zote kumzunguka.
25 Alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa akitoka damu (kama ilivyo desturi ya wanawake kila mwezi) kila siku kwa miaka kumi na miwili. 26 Huyu alikuwa ameteseka sana akiwa chini ya uangalizi wa madaktari wengi. Yeye alikuwa ametumia vyote alivyokuwa navyo. Hata hivyo hali yake iliendelea kuwa mbaya zaidi.
27 Wakati aliposikia juu ya Yesu, alimwendea kwa nyuma akiwa katika kundi lile na kuligusa joho lake. 28 Kwani alikuwa akijisemea mwenyewe, “Ikiwa nitagusa tu vazi lake, nitapona.” 29 Mara moja chanzo cha kutoka kwake damu kikakauka, na akajisikia mwilini mwake kwamba amepona matatizo yake. 30 Naye Yesu akatambua mara moja kwamba nguvu zilimtoka. Aligeuka nyuma na kuuliza “Nani aliyegusa mavazi yangu?”
31 Wanafunzi wake wakamwambia, “Uliliona kundi likisukumana kukuzunguka, nawe unauliza, Nani aliyenigusa?”
32 Lakini Yesu aliendelea kuangalia kumzunguka kuona ni nani aliyeyafanya haya. 33 Yule Mwanamke akiwa anatetemeka kwa hofu akijua nini kilichotokea kwake, alikuja na kuanguka mbele yake, akamweleza ukweli wote. 34 Kisha Yesu akamwambia, “Binti yangu imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, na uendelee kupona matatizo yako.”
35 Wakati alipokuwa akizungumza haya watumishi walikuja kutoka nyumbani kwa afisa wa sinagogi. Nao wakamwambia yule afisa, “Binti yako amefariki kwa nini uendelee kumsumbua huyo mwalimu?”
36 Lakini Yesu aliyasikia yale waliyokuwa wakisema, na akamwaambia yule afisa wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
37 Naye hakumruhusu mtu yeyote kumfuata isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, 38 nao wakaenda katika nyumba ya yule afisa wa sinagogi, na Yesu akaona vurugu na watu wakilia kwa sauti. 39 Yesu aliingia ndani na kuwaambia, “Za nini vurugu zote hizi na vilio hivi? Mtoto hajafa; amelala tu.” 40 Nao wakamcheka.
Yeye aliwatoa nje watu wote, akamchukua baba na mama wa mtoto na wale waliokuwa pamoja naye, akaenda hadi pale alipokuwepo mtoto, 41 akaushika mkono wa mtoto yule na kumwambia “Talitha koum!” (maana yake, “Msichana mdogo, ninakuambia amka usimame!”) 42 Yule msichana aliinuka mara moja na kuanza kutembea mahali pale. Naye alikuwa na miaka kumi na miwili. Nao mara moja wakaelemewa na mshangao mkubwa. 43 Yeye akawapa amri kuwa mtu yeyote asijue juu ya jambo hili. Kisha akawaambia wampatie msichana yule chakula ale.
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mt 13:53-58; Lk 4:16-30)
6 Yesu akaondoka pale, na kwenda katika mji wa kwao; na wanafunzi wake wakamfuata. 2 Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sinagogi. Watu wengi walishangazwa walipomsikiliza. Wakasema, “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Alipata wapi hekima hii? Na anaifanyaje miujiza hii inayofanyika kwa mikono yake? 3 Je, yeye si yule seremala? Je, yeye si mwana wa Maria? Je, yeye si kaka yake Yakobo, Yusufu, Yuda, na Simoni? Je, dada zake hawaishi hapa katika mji wetu?” Kulikuwa na vikwazo vilivyowazuia wasimkubali.
4 Yesu akawaambia, “kila mtu humheshimu nabii isipokuwa watu wa mji wa kwao mwenyewe, jamaa zake mwenyewe na wale wa nyumbani mwake mwenyewe.” 5 Yesu hakuweza kufanya miujiza ya aina yoyote pale, isipokuwa aliweka mikono juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6 Naye akashangazwa na jinsi watu wa mji wa kwao mwenyewe walivyokosa kuwa na imani. Kisha Yesu alizunguka vijijini akiwafundisha watu.
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake
(Mt 10:1,5-15; Lk 9:1-6)
7 Akawaita kwake wanafunzi wake kumi na wawili, na akaanza kuwatuma wawili wawili. Akawapa uwezo wa kuwaweka huru watu kutoka pepo wachafu. 8 Akawapa amri kuwa wasichukue kitu chochote kwa ajili ya safari yao isipokuwa fimbo; hawakupaswa kuchukua mkate, mfuko, hata kubeba fedha kwenye mikanda yao. 9 Aliwaruhusu kuvaa makobazi lakini wasichukue kanzu ya pili. 10 Naye akawambia, “ikiwa mtu atawapa mahali pa kuishi mkae katika nyumba hiyo kwa muda wote mtakapokuwa katika mji ule msihamehame kutoka nyumba moja hadi nyingine. 11 Ikiwa hamtakaribishwa ama kusikilizwa katika mji wowote au mahali popote, kwa kuwaonya kunguteni mavumbi toka miguuni mwenu.”
12 Kwa hiyo mitume wakatoka na kuhubiri ili watu watubu. 13 Mitume wakafukuza mashetani wengi na kuwapaka mafuta ya mizeituni[e] wagonjwa wengi na kuwaponya.
Herode Adhani Yesu ndiye Yohana Mbatizaji
(Mt 14:1-12; Lk 9:7-9)
14 Mfalme Herode alisikia habari hii kwani umaarufu wa Yesu ulikuwa umeenea mahali pote. Watu wengine walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana ana uwezo wa kufanya miujiza.”
15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”
Wengine walisema, “Yeye ni nabii kama mmoja wa manabii wa zamani.”
16 Lakini Herode aliyasikia haya na kusema, “Yohana, yule mtu niliyemkata kichwa, amefufuka kutoka kifo.”
Yohana Mbatizaji Alivyouawa
17 Kwa kuwa Herode mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kumkamata Yohana na kumweka gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mkewe Filipo kaka yake ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18 Kwani Yohana alizidi kumwambia Herode, “Si halali kwako kisheria kumwoa mke wa kaka yako.” 19 Herodia alikuwa na kisa na Yohana. Hivyo alitaka auwawe, lakini hakuweza kumshawishi Herode kumuua Yohana. 20 Hii ni kwa sababu Herode alimhofu Yohana. Herode pia alifahamu ya kuwa Yohana alikuwa ni mtu mtakatifu na mwenye haki, hivyo akamlinda. Herode alimpomsikia Yohana, alisumbuka sana; lakini alifurahia kumsikiliza.
21 Lakini muda maalumu ukafika; katika siku ya kuzaliwa kwake. Herode aliandaa sherehe ya chakula cha jioni kwa maafisa mashuhuri wa baraza lake, maafisa wake wa kijeshi, na watu maarufu wa Galilaya. 22 Binti ya Herodia alipowasili ndani ya ukumbi alicheza na kumpendeza Herode na wageni aliowaalika katika sherehe hiyo.
Mfalme Herode akamwambia yule msichana, “Uniombe chochote unachotaka, nami nitakupa.” 23 Akamuahidi: “Nitakupa chochote utakachoniomba, hata nusu ya ufalme wangu!”
24 Naye akatoka na kumwambia mama yake, “Niombe kitu gani?”
Mama yake akasema, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”
25 Yule msichana mara moja aliharakisha kuingia ndani kwa mfalme na kuomba: “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji katika sinia.”
26 Mfalme alisikitika sana. Lakini kwa sababu ya viapo vyake alivyovifanya mbele ya wageni wake chakulani hakutaka kumkatalia ombi lake. 27 Kwa hiyo mfalme mara moja akamtuma mwenye kutekeleza hukumu za kifo akiwa na amri ya kukileta kichwa cha Yohana. Kisha akaenda kukikata kichwa cha Yohana, 28 na kukileta katika sinia na kumpa yule msichana, na msichana akampa mama yake. 29 Wanafunzi wa Yohana waliposikia haya walikuja na kuchukua mwili na kuuweka ndani ya kaburi.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mt 14:13-21; Lk 9:10-17; Yh 6:1-14)
30 Mitume walikusanyika kumzunguka Yesu, na wakamweleza yote waliyofanya na kufundisha. 31 Kisha Yesu akawaambia, “Njooni mnifuate peke yenu hadi mahali patulivu na palipo mbali na watu wengine ili mpumzike kidogo”, kwani pale walikuwepo watu wengi wakija na kutoka, nao hawakuwa na nafasi ya kula.
32 Kwa hiyo wakaondoka na mtumbwi kuelekea mahali patulivu na mbali na watu wakiwa peke yao. 33 Lakini watu wengi waliwaona wakiondoka na waliwafahamu wao ni kina nani; kwa hiyo walikimbilia pale kwa njia ya nchi kavu kutoka vitongoji vyote vilivyolizunguka eneo hilo wakafika kabla ya Yesu na wanafunzi wake. 34 Alipotoka katika mashua, Yesu aliona kundi kubwa, na akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Kwa sasa ilikuwa imekwisha kuwa jioni sana. Kwa hiyo wanafunzi wake walimwijia na kusema, “Hapa ni mahali palipojitenga na sasa hivi saa zimeenda. 36 Uruhusu watu waende zao, ili kwamba waende kwenye mashamba na vijiji vinavyozunguka na waweze kujinunulia kitu cha kula.”
37 Lakini kwa kujibu aliwaambia, “Ninyi wenyewe wapeni kitu cha kula.”
Wao Wakamwambia, “Je, twende kununua mikate yenye thamani ya mshahara wa mtu mmoja[f] wa miezi minane na kuwapa wale?”
38 Yesu akawambia, “Ni mikate mingapi mliyonayo? Nendeni mkaone.”
Walienda kuhesabu, wakarudi kwa Yesu na kusema, “Tunayo mikate mitano na samaki wawili.”
39 Kisha akawaagiza wakae chini kila mmoja kwenye majani mabichi kwa vikundi. 40 Nao wakakaa kwa vikundi vya watu mia na mmoja na vya watu hamsini.
41 Akachukua ile mikate mitano na samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akashukuru na akaimega. Akawapa wanafunzi wake ili wawape watu. Pia aligawanya samaki wawili miongoni mwao wote.
42 Wakala na wote wakatosheka. 43 Wakachukua mabaki ya vipande vya mikate na samaki na kujaza vikapu kumi na viwili. 44 Na idadi ya wanaume waliokula ile mikate ilikuwa 5,000.
Yesu Atembea Juu ya Maji
(Mt 14:22-33; Yh 6:16-21)
45 Mara Yesu akawafanya wafuasi wake wapande kwenye mashua na wamtangulie kwenda Bethsaida upande wa pili wa ziwa, wakati yeye akiliacha lile kundi liondoke. 46 Baada ya Yesu kuwaaga wale watu, alienda kwenye vilima kuomba.
47 Ilipotimia jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48 Naye akawaona wanafunzi wake wakihangaika kupiga makasia, kwani upepo uliwapinga. Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi Yesu aliwaendea akitembea juu ya ziwa. Yeye akiwa karibu kuwapita, 49 wanafunzi wake wakamwona akitembea juu ya ziwa,[g] na wakafikiri kuwa alikuwa ni mzimu, ndipo walipopiga kelele. 50 Kwa kuwa wote walimwona, na wakaogopa. Mara tu alizungumza nao na kuwaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Usiogope.” 51 Kisha alipanda kwenye mtumbwi pamoja nao, na upepo ukatulia. Wakashangaa kabisa, 52 kwa kuwa walikuwa bado hawajauelewa ule muujiza wa mikate. Kwani fahamu zao zilikuwa zimezibwa.
Yesu Awaponya Watu Wengi Wagonjwa
(Mt 14:34-36)
53 Walipolivuka ziwa, walifika Genesareti na wakaifunga mashua. 54 Walipotoka katika mashua, watu wakamtambua Yesu, 55 Wakakimbia katika lile jimbo lote na kuanza kuwabeba wagonjwa katika machela na kuwapeleka pale waliposikia kuwa Yesu yupo. 56 Na kila alipoenda vijijini, mijini na mashambani, waliwaweka wagonjwa kwenye masoko, na wakamsihi awaache waguse pindo la koti lake. Na wote walioligusa walipona.
Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu
(Mt 15:1-20)
7 Mafarisayo na baadhi ya walimu wa Sheria waliokuja kutoka Yerusalemu walikusanyika mbele zake. 2 Hao wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula chao kwa mikono michafu (yaani bila kuosha mikono yao). 3 Kwani Mafarisayo na Wayahudi wengineo wote hawawezi kula isipokuwa wameosha mikono yao kwa njia maalumu, kulingana na desturi ya wazee. 4 Na wanaporudi kutoka sokoni, hawali chakula kwanza mpaka wamenawa. Na zipo desturi nyingi wanazozishika, kama vile kuosha vikombe, magudulia na mitungi ya shaba.[h]
5 Kwa hiyo Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, badala yake wanakula chakula chao kwa mikono isiyo safi?”
6 Yesu akawaambia, “Isaya alikuwa sahihi alipotoa unabii juu yenu enyi wanafiki, kama ilivyoandikwa:
‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
7 Ibada wanayonitolea haifai,
kwa sababu wanawafundisha watu amri
zilizotungwa na wanadamu kana kwamba ndizo itikadi zao.’(A)
8 Mmezipuuza amri za Mungu, na mnashikilia desturi za binadamu.”
9 Yesu akawaambia, “Ninyi ni wazuri katika kuzikataa amri za Mungu ili kuanzisha desturi yenu. 10 Kwa mfano Musa alisema, ‘Mheshimu baba yako na mama yako,’(B) na yule mtu atakayesema maneno mabaya juu ya ‘mama au baba yake itampasa auwawe.’(C) 11 Lakini ikiwa mtu atamwambia baba au mama yake, ‘Nilikuwa na kitu ambacho ningekupa kikusaidie, lakini nimeahidi kukitoa wakfu kwa Mungu, nacho sasa ni kurbani.[i]’ 12 Kisha, anasema, hivyo hawezi kufanya kitu chochote kwa ajili ya kumsaidia baba au mama yake. 13 Kwa hiyo unalifanya neno la Mungu kuwa batili kwa desturi mlizozirithishana. Na mnafanya mambo mengi mengine yanayofanana na hayo.”
14 Yesu akaliita lile kundi kwake na kuwaambia, “Kila mmoja anisikilize na kunielewa. 15 Hakuna kitu kilicho nje ya mtu kinachoweza kumchafua kwa kumwingia. Lakini vitu vinavyotoka ndani ya mtu ndivyo vinavyomchafua.” 16 [j]
17 Na alipoliacha lile kundi na kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza juu ya fumbo lile. 18 Na akawaambia, “Hata nanyi hamuelewi pia? Je, hamuelewi ya kuwa hakuna kinachomwingia mtu kutoka nje kinachoweza kumchafua mtu? 19 Kwa sababu hakiingii ndani ya moyo wake bali kinaenda tumboni mwake na kasha kinatoka na kwenda chooni.” Kwa kuyasema hayo alivifanya vyakula vyote kuwa safi.
20 Na Yesu akasema, “Ni kile kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomchafua. 21 Kwani mambo hayo yote mabaya hutoka ndani ya moyo wa mwanadamu; yaani mawazo mabaya na uasherati, wizi, mauaji, 22 zinaa, ulafi, kufanya mabaya kwa watu, udanganyifu, kufanya uhuni, wivu, kutukana, kujivuna, na ujinga. 23 Mambo haya yote yanatoka ndani ya mtu nayo ndiyo yanayomfanya asikubalike kwa Mungu.”
Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi
(Mt 15:21-28)
24 Yesu akaondoka mahali pale na kuenda katika eneo lililozunguka Tiro. Aliingia katika nyumba na hakutaka mu yeyote ajue hilo, lakini hakuweza kufanya siri kuwepo kwake. 25 Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo mchafu mara moja akasikia juu ya Yesu hivyo alimwijia na kuanguka chini yake. 26 Mwanamke huyo alikuwa ni Mgiriki na siyo Myahudi, na alikuwa amezaliwa Foeniki ya Shamu. Yeye alimsihi amfukuze pepo yule kutoka kwa binti yake.
27 Yesu akamwambia, “Kwanza waache watoto watosheke, kwani sio haki kuwanyanganya watoto mkate wao na kuwapa mbwa.”
28 Lakini yeye akajibu, “Bwana hata mbwa walio chini ya meza wanakula mabaki ya chakula cha watoto.”
29 Kisha Yesu akamwambia, “kwa majibu haya unaweza kwenda nyumbani kwa amani: pepo mbaya amekwisha mtoka binti yako.”
30 Kwa hiyo akaenda nyumbani na akamkuta amelala akipumzika kitandani, na yule pepo tayari amekwisha mtoka.
Yesu Amponya Asiyesikia
31 Yesu akarudi kutoka katika eneo kuzunguka jiji la Tiro na akapita katika jiji la Sidoni hadi Ziwa Galilaya akipita katika jimbo la Dekapoli. 32 Pale watu wengine wakamletea mtu asiyeweza kusikia na tena aliyesema kwa shida. Nao wakamwomba Yesu amwekee mikono yake na kumponya.
33 Yesu akamchukua pembeni, kutoka katika kundi, na akaweka vidole vyake ndani ya masikio yake. Kisha Yesu akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34 Akaangalia juu mbinguni, akapumua na kumwambia “Efatha” yaani, “Funguka!” 35 Mara masikio ya mtu yule yakafunguka, na ulimi wake ukawa huru, na akaanza kuzungumza, vizuri.
36 Lakini kadiri jinsi alivyowaamuru wasimwambie mtu ndivyo walivyozidi kueneza habari hiyo. 37 Na watu wakashangazwa kabisa na kusema, “Yesu amefanya kila kitu vyema. Kwani amewafanya wale wasiosikia kusikia na wasiosema kusema.”
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000
(Mt 15:32-39)
8 Wakati mwingine katika siku zile kundi kubwa la watu lilikusanyika na halikuwa na chakula. Yesu akawaita wanafunzi wake na kuwaambia, 2 “Nawahurumia watu hawa, kwa sababu hata sasa wamekuwa nami kwa siku tatu, na hawana kitu cha kula.”
3 Nikiwaacha waende majumbani mwao wakiwa na njaa, wataanguka njiani; na baadhi yao wametoka mbali.
4 Wanafunzi wake wakamjibu, “Wapi mtu yeyote atapata chakula cha kutosha mahali hapa jangwani cha kuwalisha watu hawa?”
5 Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakajibu, “Saba.”
6 Kisha Yesu akaliagiza kundi la watu kuketi chini ardhini Akachukua mikate ile saba, akashukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake waigawe. Nao wakaigawa kwenye kundi. 7 Kulikuwapo pia samaki wadogo wachache. Yesu akawabariki wale samaki na kuwaambia waigawe nayo pia.
8 Watu walikula na kushiba. Wakakusanya vikapu saba vilivyojaa mabaki. 9 Ilikuwa kama watu 4,000. Kisha Yesu akawaacha waende. 10 Mara Yesu akapanda katika mashua na wanafunzi wake, na akafika katika wilaya ya Dalmanutha.
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mt 16:1-4; Lk 11:16,29)
11 Mafarisayo wakamwendea Yesu na kuanza kubishana naye. Ili kumjaribu wakamwomba ishara kutoka mbinguni. 12 Yesu alihema kwa nguvu na kusema, “Kwa nini kizazi kinataka ishara? Ninawaambia ukweli: hakuna ishara itakayooneshwa kwa kizazi hiki.” 13 Kisha Yesu akawaacha, akapanda tena katika mashua, na akaondoka kwenda upande wa pili wa ziwa.
Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu
(Mt 16:5-12)
14 Wakati huo huo wanafunzi walikuwa wamesahau kuleta mikate yo yote, na hawakuwa na kitu kingine isipokuwa mkate mmoja. 15 Yesu akawaonya, akasema, “Mwe mwangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ile ya Herode.”
16 Nao wakaanza kujadiliana haya miongoni mwao: “Labda alisema hivi kwa sababu hatukuwa na mkate wowote.”
17 Akijua walichokuwa wakikisema, akawaambia, “Kwa nini mnajadiliana juu ya kutopata mkate? Je! Bado hamwoni na kuelewa? Je! Mmezifunga akili zenu. 18 Mnayo macho; Je! Hamwoni? Mnayo masikio; Je! Hamwezi kusikia? Mnakumbuka? 19 Nilipomega na kugawa mikate mitano kwa watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”
Wakasema “Kumi na viwili”.
20 “Nilipomega na kugawa mikate saba kwa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”
Wakasema “Saba”.
21 Kisha akawaambia, “Bado hamwelewi?”
Yesu Amponya Kipofu katika Kijiji cha Bethsaida
22 Walipofika katika kijiji cha Bethsaida, baadhi ya watu walimleta asiyeona kwa Yesu, na kumsihi Yesu amguse. 23 Yesu alimshika mkono yule asiyeona na kumtoa nje ya kijiji. Kisha Yesu alimtemea mate yule asiyeona kwenye macho yake, akaweka mkono wake juu ya asiyeona, na kumwuliza, “Je! Unaona kitu chochote?”
24 Kipofu akatazama juu na kusema, “Ninaona watu; wanaonekana kama miti inayotembea.”
25 Kisha Yesu akaweka mikono yake tena kwenye macho ya yule asiyeona. Naye akafumbua wazi macho yake yote. Kwani alipona kutokuona kwake na kuona kila kitu kwa uwazi. 26 Kisha Yesu akamwambia arudi nyumbani, na pia akamwambia, “Usiingie kijijini.”
Petro Atambua Yesu ni Nani
(Mt 16:13-20; Lk 9:18-21)
27 Yesu na wanafunzi wake walikwenda kwenye vijiji vinavyozunguka Kaisaria Filipi. Wakiwa njiani aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?”
28 Nao wakamjibu, “Yohana Mbatizaji. Wengine husema wewe ni Eliya. Na wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.”
29 Kisha akawauliza wao, “Na ninyi; Je! Mnasema mimi ni nani?”
Petro akamjibu, “Wewe ni masihi.”
30 Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote kuhusu yeye.
Yesu Asema ni Lazima Afe
(Mt 16:21-28; Lk 9:22-27)
31 Ndipo alianza kuwafundisha akisema: “Mwana wa Adamu lazima apate mateso mengi, na kukatataliwa na wazee, wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria, na ni lazima atauawa na Kufufufuka baada ya siku ya tatu.” 32 Yesu aliwaambia haya kwa uwazi bila kuwaficha.
Baada ya mafundisho haya Petro alimchukua Yesu pembeni na kuanza kumkemea. 33 Lakini Yesu aligeuka nyuma na kuwaangalia wanafunzi wake, na kumkemea Petro kwa kumwambia, “Shetani,[k] toka mbele yangu! Huyajali yale anayoyajali Mungu bali yale wanayoyaona wanadamu kuwa ni muhimu.”
34 Kisha Yesu akaliita kundi lote pamoja na wanafunzi wake kwake, akawaambia, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, lazima ajikane yeye mwenyewe, na ni lazima auchukue msalaba wake mwenyewe kisha anifuate. 35 Kwa kuwa kila anayetaka kuusalimisha uhai wake, ataupoteza, na yeyote atakayeupoteza uhai wake kwa ajili yangu na kwa ajili ya injili atausalimisha. 36 Itampa mtu manufaa gani akiupata ulimwengu wote kisha akaupoteza uhai wake? 37 Mtu anaweza kuubadilisha uhai wake na kitu gani? 38 Hiki ni kizazi chenye dhambi na kisichokuwa na uaminifu. Hivyo, mtu yeyote atakayenionea haya mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea haya mtu huyo siku ile atakaporudi katika utukufu wa Baba yake akiwa na malaika wake watakatifu.”
9 Naye Yesu aliwaambia, “Ninawaambia Ukweli: baadhi yenu mnaosimama hapa mtauona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu kabla ya kufa kwenu.”
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mt 17:1-13; Lk 9:28-36)
2 Baada ya siku sita, Yesu akamchukua Petro, Yakobo na Yohana na kuwaongoza hadi mlima mrefu wakiwa peke yao tu. Na mwonekano wa Yesu ulibadilika mbele yao. Huko Yesu akabadilika sura nyingine akiwa mbele yao. 3 Mavazi yake yakiwa na mng'ao, na meupe kabisa kuliko mtu anavyoweza kufua nguo kwa sabuni na kuitakatisha. 4 Huko Eliya na Musa pia wakawatokea, na Yesu alizungumza na manabii hao wawili.
5 Petro akafungua kinywa chake na kumwambia Yesu, “Mwalimu, ni vyema tupo hapa. Tufanye basi vibanda vitatu; moja kwa ajili yako, moja kwa ajili ya Musa na moja kwa ajili ya Eliya.” 6 Petro aliyasema haya kwa sababu hakujua aseme nini, kwa sababu yeye na wenzake walikuwa wamepata hofu.
7 Ndipo wingu likaja na kuwafunika wote kwa kivuli chake. Na sauti ikatoka mawinguni, ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa. Msikilizeni yeye.”
8 Ndipo ghafula walipokuwa wakiangalia huku na huko, hawakuona mtu yeyote akiwa pamoja nao isipokuwa Yesu peke yake.
9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote kile walichokiona mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka katika wafu.
10 Hivyo hawakuwaeleza wengine juu ya jambo lile bali walijadiliana miongoni mwao wenyewe juu ya maana ya “kufufuka kutoka kwa wafu.” 11 Wakamwuliza Yesu, “kwa nini walimu wa sheria wanasema Eliya lazima aje kwanza?”
12 Yesu akawaambia, “Ndiyo, Eliya atakuja kwanza[l] kuja kuyaweka mambo yote sawa kama jinsi yalivyokuwa hapo mwanzo. Lakini kwa nini imeandikwa juu ya Mwana wa Adamu[m] ya kwamba itampasa kuteswa na kudhalilishwa? 13 Lakini ninawaambia, Eliya amekuja,[n] na walimtendea kila kitu walichotaka, kama vile ilivyoandikwa[o] kuhusu yeye.”
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mt 17:14-20; Lk 9:37-43a)
14 Wakati Yesu, Petro, Yakobo, na Yohana walipowafikia wanafunzi wengine, waliliona kundi kubwa la watu lililowazunguka na wakawaona walimu wa Sheria wakibishana nao. 15 Mara tu watu wote walipomwona Yesu, walishangazwa, na wakakimbia kwenda kumsalimia.
16 Akawauliza, “Mnabishana nao kitu gani?”
17 Na mtu mmoja kundini alimjibu, “Mwalimu, nilimleta mwanangu kwako ili umponye. Yeye amefungwa na pepo mbaya anayemfanya asiweze kuzungumza. 18 Na kila mara anapomshambulia humtupa chini ardhini. Naye hutokwa mapovu mdomoni na kusaga meno yake, huku akiwa mkakamavu. Nami niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze kutoka ndani yake, lakini hawakuweza.”
19 Kisha Yesu akajibu na kuwaambia, “ninyi kizazi kisichoamini, kwa muda gani niwe pamoja nanyi? Kwa muda gani nitapaswa kuchukuliana nanyi? Mleteni huyo mvulana kwangu.”
20 Wakamleta yule mvulana kwake. Na yule pepo alipomwona Yesu, kwa ghafula akamtingisha yule mvulana ambaye alianguka chini kwenye udongo, akivingirika na kutokwa povu mdomoni.
21 Yesu akamwuliza babaye, “Kwa muda gani amekuwa katika hali hii?”
Yule babaye akajibu akisema, “amekuwa katika hali hii tangu utoto. 22 Mara nyingi anamtupa katika moto ama katika maji ili kumwua. Lakini ikiwa unaweza kufanya kitu chochote, uwe na huruma na utusaidie.”
23 Yesu akamwambia, “Una maana gani kusema ‘ikiwa unaweza’? Kila kitu kinawezekana kwake yeye anayeamini.”
24 Mara, babaye yule mvulana alilia kwa sauti kubwa na kusema, “Naamini! Nisaidie kutokuamini kwangu.”
25 Yesu alipoona lile kundi likizidi kuwa kubwa, alimkemea yule pepo mchafu na kumwambia, “Wewe pepo uliyemfanya mvulana huyu asiweze kusikia na asiweze kusema, nakuamuru, utoke ndani yake, na usimwingie tena!”
26 Na pepo yule alilia kwa sauti, akamtupa yule mvulana chini katika mishituko ya kutisha, kisha akatoka, naye akawa kama mtu aliyekufa, kiasi kwamba watu wengi wakadhani ya kuwa amekufa. 27 Lakini Yesu akamshika yule mvulana mikononi, na kumwinua naye akasimama.
28 Baada ya Yesu kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuuliza wakiwa peke yao, “Kwa nini sisi hatukuweza kumfukuza pepo yule?”
29 Naye akawaambia, “Aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa maombi.”[p]
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mt 17:22-23; Lk 9:43-45)
30 Wakaondoka mahali pale na kusafiri kupitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu yeyote kujua walikuwa huko, 31 alitaka kuwafundisha wanafunzi wake peke yake. Na Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kuwekwa mikononi mwa watu wengine, nao watamwua. Kisha siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32 Lakini hawakuuelewa usemi huu, na walikuwa wanaogopa kumuuliza zaidi.
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mt 18:1-5; Lk 9:46-48)
33 Kisha wakaja Kapernaumu. Na Yesu alipokuwa ndani ya nyumba aliwauliza, “Je, mlikuwa mnajidiliana nini njiani?” 34 Lakini wao walinyamaza kimya, kwa sababu njiani walikuwa wamebishana juu ya nani kati yao alikuwa ni mkuu zaidi.
35 Hivyo Yesu aliketi chini, akawaita wale kumi na mbili, na akawaambia, “Ikiwa yupo mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, inapasa basi awe wa mwisho kuliko wote na mtumishi wa wote.”
36 Akamchukua mtoto mdogo mikononi mwake na kumsimamisha mbele yao. Akimkumbatia mtoto huyo, Yesu alisema, 37 “Yeyote atakayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu hapa kwa sababu ya jina langu basi ananikaribisha na mimi pia. Yeyote anayenikubali mimi hanikubali mimi tu bali anamkubali pia yeye aliyenituma.”
Yeyote Ambaye Hayuko Kinyume Chetu Yuko Pamoja Nasi
(Lk 9:49-50)
38 Yohana akamwambia Yesu, “Mwalimu tulimwona mtu akifukuza pepo kwa jina lako. Nasi tulijaribu kumzuia, kwa sababu hakuwa mmoja wetu.”
39 Lakini Yesu akawaambia, “Msimzuie, kwa sababu hakuna atendaye miujiza kwa jina langu kisha mara baada ya hilo aseme maneno mabaya juu yangu. 40 Yeye ambaye hapingani na sisi basi yuko pamoja na sisi. 41 Yeyote anayewapa ninyi kikombe cha maji kwa sababu ninyi ni wake Kristo.[q] Hakika ninawaambia ukweli kwamba, hatapoteza thawabu yake.
Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi
(Mt 18:6-9; Lk 17:1-2)
42 Yeyote anayemsababisha mmoja wa hawa walio wadogo ambao wananiamini mimi kujikwaa na kuanguka, itakuwa bora kwake ikiwa atatupwa baharini huku amefungwa jiwe la kusagia shingoni mwake. 43 Ikiwa mkono wako unakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili na kuenda Jehanamu, ambako kuna moto usiozimika. 44 [r] 45 Na ikiwa mguu wako utakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa mlemavu kuliko kuwa na miguu miwili na kutupwa Jehanamu. 46 [s] 47 Na kama jicho lako litakusababisha ufanye dhambi, liondoe. Ni bora uingie katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja kuliko kuwa nayo macho mawili na kutupwa Jehanamu, 48 ambapo waliomo watatafunwa na funza wasiokufa na kuchomwa na moto usiozimika kamwe.(D)
49 Kwa kuwa kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.[t]
50 Chumvi ni njema. Lakini ikiwa chumvi itaharibika, utawezaje kuifanya chumvi tena? Muwe na chumvi miongoni mwenu na muishi kwa amani ninyi kwa ninyi.”
Yesu Afundisha Kuhusu Talaka
(Mt 19:1-12)
10 Naye aliondoka mahali pale, na kufika katika nchi ya Uyahudi ng'ambo ya Mto Yordani. Na makundi ya watu wakamjia tena na kama alivyofanya daima aliwafundisha.
2 Kisha baadhi ya Mafarisayo walimwendea na kumwuliza “Je, ni sahihi mtu kumtaliki mkewe?” Nao walimwuliza hivyo ili kumjaribu.
3 Yesu akawajibu, “Musa aliwapa amri mfanye nini?”
4 Wakasema, “Musa alimpa ruhusa mume kuandika hati ya kutangua ndoa[u] na kisha kumtaliki mke wake.”
5 Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia amri hii kwa sababu ninyi ni wakaidi na hamkutaka kuyapokea mafundisho ya Mungu. 6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji wake Mungu ‘aliwaumba mwanaume na mwanamke’.(E) 7 ‘Basi kwa sababu ya hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, na kujiunga na mkewe. 8 Na hao wawili wataungana pamoja na kuwa mwili mmoja.’(F) Nao si wawili tena bali ni mwili mmoja. 9 Kwa hiyo, mtu yeyote asitenganishe kile ambacho Mungu amekiunganisha pamoja.”
10 Walipokuwa ndani ya nyumba ile kwa mara nyingine, wanafunzi wake wakamwuliza Yesu juu ya jambo hili. 11 Naye akawaambia, “yeyote atakayemtaliki mke wake na kuoa mwanamke mwingine, anazini kinyume cha mkewe. 12 Na ikiwa mke atamtaliki[v] mumewe na kuolewa na mume mwingine, basi naye anafanya zinaa.”[w]
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mt 19:13-15; Lk 18:15-17)
13 Nao watu wakawaleta watoto wadogo kwa Yesu, ili aweze kuwawekea mikono na kuwabariki. Hata hivyo wanafunzi wake waliwakemea. 14 Yesu alipoona hayo, alikasirika, na akawaambia, “Waruhusuni watoto hao waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu kama hao. 15 Ninawaambia kweli, Yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyoupokea hataweza kuingia ndani yake.” 16 Naye Yesu akawakumbatia watoto kifuani mwake na akaweka mikono yake juu yao na kuwabariki.
Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu
(Mt 19:16-30; Lk 18:18-30)
17 Na alipokuwa ameanza safari, mtu mmoja alimkimbilia, akafika na kupiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?
18 Yesu akamwuliza, kwa nini unaniita mimi mwema? Hakuna aliye mwema isipokuwa Mungu peke yake. 19 Je, unazijua amri: Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo, usidanganye wengine, uwaheshimu baba na mama yako.”(G)
20 Naye akamwambia Yesu, “Mwalimu, nimeyatii hayo tangu ujana wangu.”
21 Yesu akamwangalia. Naye akashikwa na upendo kwa mtu yule, na hivyo akamwambia, “umekosa kitu kimoja: Nenda ukaviuze vyote ulivyo navyo kisha ukawape walio maskini, nawe utakuwa umejitunzia hazina mbinguni. Kisha uje ukanifuate.”
22 Yule mtu alisikitishwa sana na usemi huo, na akaondoka kwa huzuni kwa kuwa alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu aligeuka kuwatazama wanafunzi wake na kuwaambia wake, “Angalieni jinsi ilivyo vigumu sana kwa walio na mali nyingi kuingia katika ufalme wa Mungu.”
24 Wanafunzi wake walistaajabishwa na maneno yale. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, ni vigumu[x] sana kuuingia ufalme wa Mungu. 25 Kwani ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuuingia ufalme wa Mungu.”
26 Nao walistajaabu zaidi, na wakaambiana wao kwa wao, “Ni nani basi atakayeweza kuokolewa?”
27 Huku akiwatazama, Yesu alisema, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, lakini kwa Mungu linawezekana, kwa sababu yote yanawezekana kwake Mungu.”
28 Petro akaanza kumwambia, “Tazama! Tumeacha kila kitu tukakufuata.”
29 Yesu akasema, “Nawaambieni kweli: Hakuna aliyeacha nyumba, kaka, dada, mama, baba, watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili 30 ambaye hatapata malipo mara mia zaidi katika nyakati hizi; nyumba, kaka, dada, mama, watoto, na mashamba, pamoja na mateso; na uzima wa milele katika kizazi kinachokuja. 31 Lakini wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho baadaye na wale walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza baadaye.”
Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake
(Mt 20:17-19; Lk 18:31-34)
32 Walikuwa wote njiani wakipanda kuelekea Yerusalemu, na Yesu alikuwa akitembea mbele yao. Nao walisumbuka sana. Na wale waliowafuata walikuwa na hofu pia. Kwa mara nyingine Yesu akawachukua wale wanafunzi kumi na mbili pembeni, na akaanza kuwaeleza yale yatakayomtokea Yerusalemu. 33 “Sikilizeni! Tunaelekea hadi Yerusalemu na Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria, nao watamtia hatiani na kumpa hukumu kifo, kisha watamtoa kwa wale wasio Wayahudi, 34 Nao watamdhihaki, na watamtemea mate, na watamchapa kwa viboko vya ngozi, nao watamwua. Ndipo atafufuka baada ya siku ya tatu.”
Yakobo na Yohana Waomba Kutawala Pamoja na Yesu
(Mt 20:20-28)
35 Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu, wakamwambia, “Mwalimu tunataka utufanyie kile tunachokuomba.”
36 Yesu akawaambia, “Ni kitu gani mnachotaka niwafanyie?”
37 Nao wakamwambia, “Uturuhusu tuketi pamoja nawe katika utukufu wako, mmoja wetu aketi kulia kwako na mwingine kushoto kwako.”
38 Yesu akawaambia, “Hamjui mnachokiomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninachokinywea[y] mimi? Au mnaweza kubatizwa ubatizo ninaobatizwa?”
39 Wakamwambia, “Tunaweza.”
Kisha Yesu akawaambia, “Mtakinywa kikombe cha mateso ninachokunywa mimi, na mtabatizwa ubatizo[z] ninaobatizwa mimi. 40 Lakini kuhusu kuketi kulia kwangu ama kushoto kwangu siyo mamlaka yangu kusema. Mungu ameandaa nafasi hizo kwa ajili ya wale aliowateuwa.”
41 Wale wanafunzi kumi wengine walipoyasikia maombi haya, waliwakasirikia Yakobo na Yohana. 42 Na Yesu akawaita wale wanafunzi kumi na kusema, “Mnajua kuwa miongoni mwa mataifa watawala huwa na mamlaka makubwa juu ya watu, na viongozi wenye nguvu huwakandamiza watu wao. 43 Haipaswi kuwa hivyo miongoni mwenu. Kwani yeyote atakaye kuwa mkuu miongoni mwenu basi na awe mtumishi wenu. 44 Yeyote anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima akubali kuwa mtumwa wenu wote. 45 Kwani hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa bali alikuja kuwatumikia wengine na kuyatoa maisha yake ili kuwaweka huru wengi.”
Yesu Amponya Asiyeona
(Mt 20:29-34; Lk 18:35-43)
46 Kisha wakafika Yeriko. Yesu alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati wa watu, Bartimayo mwana wa Timayo, ombaomba asiyeona, alikuwa amekaa kando ya barabara. 47 Aliposikia kwamba huyo alikuwa ni Yesu wa Nazareti, alianza kupiga kelele na kusema, “Yesu Mwana wa Daudi, unihurumie!”
48 Na watu wengi walimkemea na kumwambia anyamaze kimya. Lakini yeye alipiga kelele kwa sauti kubwa zaidi na kusema, “Mwana wa Daudi, unihurumie!”
49 Kwa hiyo Yesu akasimama na kusema, “Hebu mwiteni.”
Nao wakamwita yule mtu asiyeona na kumweleza, “Jipe moyo mkuu! Inuka! Yesu anakuita.” 50 Naye akalitupa joho lake, akaruka juu, na akamwendea Yesu.
51 Naye Yesu akamwambia, “Unataka nikufanyie nini?”
Yule mtu asiyeona akamwambia, “Mwalimu, nataka kuona tena.”
52 Hivyo Yesu akamwambia, “Nenda! Imani yako imekuponya.”[aa] Na mara akaweza kuona tena, na akamfuata Yesu barabarani.
Footnotes
- 5:1 Wagerasi Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagadarini” na zingine zimewaita “Wagergesini”.
- 5:9 Jeshi Jina hili lina maana nyingi sana. Jina hili lina maana “wengi zaidi” Ni neno lililotumika kwa kundi la wanajeshi 6,000 wa Jeshi la Kirumi.
- 5:13 nguruwe Watu kijijini walikuwa wakiwatunza nguruwe katika kundi moja kubwa. Kundi hilo lilikuwa chanzo muhimu cha mapato kwa kijiji.
- 5:20 Dekapoli Eneo wanaloishi wasio Wayahudi mashariki mwa Galilaya inaloitwa pia Eneo la Miji Kumi.
- 6:13 kuwapaka mafuta ya mizeituni Mafuta ya mizeituni yalitumika kama dawa. Ilikuwa pia ni alama ya uponyaji wa Mungu aliopewa Yesu na baadaye wanafunzi wake na Roho Mtakatifu.
- 6:37 thamani ya mshahara wa mtu mmoja Kwa Kiyunani vipande 200 vya fedha vimelinganishwa na TKU kama kiasi cha mshahara wa mtu mmoja kwa miezi minane.
- 6:49 akitembea juu ya ziwa Watu zama za Marko waliamini kwamba mizimu isingeweza kutembea juu ya maji, lakini waliamini miungu wangeweza kutembea juu ya maji. Watu hao wangeshangaa kuona mitume wa Yesu wakiwa tayari kuamini kitu potovu kabla ya kuamini kuwa Yesu alisimama mbele yao ni Mungu kwani ametembea majini.
- 7:4 mitungi ya shaba Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza “na makochi”.
- 7:11 kurbani Yaani zawadi ama sadaka iliyotolewa kwa Mungu.
- 7:16 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 16: “Kila mwenye masikio ya kusikilia na asikilize.”
- 8:33 Shetani Jina la Mwovu lenye maana “Adui”. Maana ya Yesu ni kuwa Petro alikuwa akiongea kama Shetani.
- 9:12 atakuja kwanza Ama atatangulia.
- 9:12 Mwana wa Adamu Jina lingine alilojitambulisha Yesu.
- 9:13 Eliya amekuja Habari hii inamhusu Yohana Mbatizaji.
- 9:13 kama vile ilivyoandikwa Hii inahusu maandiko ya Agano la Kale.
- 9:29 maombi Nakala zingine za Kiyunani zina “maombi na kufunga”.
- 9:41 Kristo Mpakwa mafuta au masihi, aliyechaguliwa na Mungu.
- 9:44 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza mstari wa 44, ambao ni sawa na mstari 48.
- 9:46 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza mstari wa 46, ambao ni sawa na mstari 48.
- 9:49 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza, “Kila dhabihu itatiwa chumvi.” Katika Agano la Kale chumvi ilinyunyiziwa kwenye dhabihu. Mstari huu unaweza kuwa na maana kuwa wanafunzi wa Yesu watajaribiwa kwa mateso na kwamba wanapaswa kujitoa wenyewe kwa Mungu kama dhabihu.
- 10:4 hati ya kutangua ndoa Ama talaka 24:1.
- 10:12 atamtaliki Ama kumwacha yaani kutoa talaka. Pia kutaliki ni kutoa talaka, ambayo ni kuandika hati ya kutangua ndoa (tazama mstari 4 hapo juu).
- 10:12 zinaa Zinaa ni Kuvunja ahadi ya ndoa kwa kufanya dhambi ya mtu kulala na mtu mwingine asiye mume ama mkewe wa ndoa.
- 10:24 vigumu Baadhi ya nakala za zamani za Kiyunani zina “vigumu kwa wale walioweka matumaini yao kwenye utajiri”.
- 10:38 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao.
- 10:39 ubatizo Neno hili ubatizo lina maana ya kutumbukiza majini, lakini pia lina maana maalumu hapa, ambayo ni kufunikwa, kuwekwa ndani ya ama kufunikwa au kuzikwa mwili wote.
- 10:52 imekuponya Kiyunani kinatumia neno hilo hilo kuwa na maana ya neno kuponya na kumaanisha kuokoa.
© 2017 Bible League International