Add parallel Print Page Options

Kufuata Mafundisho ya Kweli

Lakini wewe Tito daima uwaambie waaminio mambo yanayokubaliana na mafundisho ya kweli na yenye uzima. Wanaume wazee wanapaswa kuwa na kiasi na kufanya mambo yenye kuleta heshima. Wanapaswa kuwa na busara katika maisha yao. Kuwa na nguvu katika imani kwa Mungu, upendo kwa wengine, na uvumilivu.

Vivyo hivyo wafundishe wanawake wazee wawe na mwenendo mzuri. Wafundishe wasiwe wachochezi na wasiwe watumwa wa mvinyo. Wanapaswa kufundisha yale yaliyo mema. Kwa jinsi hiyo wataweza kuwakumbusha wanawake vijana jinsi wanavyopaswa kuishi. Wanawake vijana wanapaswa kuwaonesha upendo waume zao na kuwapenda watoto wao. Wanapaswa kuwa na busara na wasafi kiroho, wakizitunza nyumba zao, kuwa wakarimu, na kuwa tayari kuwatumikia waume zao wenyewe, ili asiwepo atakayeudharau ujumbe wa Neno la Mungu.

Kadhalika endelea kuwahimiza wanaume vijana kuwa na busara. Katika kila kitu ujioneshe kuwa wewe ni mfano wa matendo mema. Katika mafundisho yako onesha kuwa una moyo safi na uko makini. Ufundishe kile ambacho ni sahihi kwa wazi, ili asiwepo yeyote atakayepinga mafundisho yako. Tumia mazuri ambayo hayatasemwa vibaya ili wale wanaokupinga waaibishwe kwa ajili ya kukosa lo lote baya la kusema dhidi yetu.

Wafundishe watumwa kuwatii bwana zao katika kila jambo, wajitahidi kuwapendeza na sio kubishana nao 10 wala kwa siri wasiwaibie bali waudhihirishe uaminifu kamili, ili katika mambo yote wayapatie sifa njema mafundisho kutoka kwa Mungu, Mwokozi wetu.

11 Maana Mungu ameidhihirisha neema yake inayookoa kwa watu wote. 12 Hiyo inatufundisha kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia ili tuishi katika ulimwengu wa sasa kwa njia ya werevu, haki na kuionesha heshima yetu kwa Mungu, 13 kadri tunavyosubiri ile Siku iliyobarikiwa tunayoitumaini ambapo utukufu wa Mungu wetu mkuu na Mwokozi Yesu Kristo itakapofunuliwa. 14 Alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili aweze kutuweka huru sisi kutoka katika uovu wote na kuweza kutusafisha kwa ajili yake watu walio wake mwenyewe, wale walio na shauku ya kufanya matendo mema.

15 Endelea kufundisha ukihimiza na kukemea kuhusu mambo haya, na fanya hivyo kwa mamlaka yote, na mtu yeyote asikudharau.

Kutoka kwa Paulo mfungwa kwa kusudi la Kristo Yesu,[a] na kutoka kwa Timotheo ndugu yetu. Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtenda kazi pamoja nasi; kwa Afia dada yetu, Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa linalokutania nyumbani mwako.

Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo ziwe pamoja nawe.

Upendo na Imani ya Filemoni

Namshukuru Mungu wangu siku zote kila ninapokukumbuka katika maombi yangu, kwa sababu nasikia juu ya upendo na uaminifu ulionao katika Bwana Yesu na unaouonesha kwa watu wa Mungu. Ninaomba kwamba ile imani unayoishiriki pamoja nasi ikusaidie wewe kuelewa kila fursa tulio nayo ya kutenda mema kama wale tunaomwamini Kristo. Nimepokea furaha kubwa na faraja kutokana na upendo wako, kwa sababu mioyo ya watu wa Mungu imepata nguvu mpya kwa juhudi zako ndugu yangu.

Mpokee Onesimo Kama Kaka

Hivyo hiyo ndiyo sababu nakuagiza wewe kufanya jambo unalopaswa kulifanya. Kwa mamlaka niliyo nayo katika Kristo naweza kukuamuru kufanya hilo. Lakini sikuamuru; bali kwa sababu ya upendo nakusihi ufanye hivyo. Mimi Paulo, niliye mzee wa umri sasa, na sasa mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu. 10 Ninakusihi kuhusu mwanangu Onesimo niliyemleta[b] katika maisha mapya tulio nayo katika Bwana nilipokuwa gerezani. 11 Huyo ambaye siku za nyuma hakuwa wa manufaa kwako, lakini sasa anafaa[c] sio kwako tu bali hata kwangu mimi.

12 Ninamrudisha kwako, kitu ambacho kimekuwa kigumu sawa na kuupoteza moyo wangu.[d] 13 Ningetamani kuendelea kuwa naye hapa, ili aendelee kunihudumia kwa niaba yako nitakapokuwa bado gerezani kwa ajili ya Habari Njema. 14 Lakini sikuwa tayari kufanya jambo lo lote bila ruhusa yako, ili kila jambo lako zuri litendeke bila lazima bali kwa hiari yako mwenyewe.

15 Labda sababu ya Onesimo kutenganishwa nawe kwa kipindi kifupi ni kuwezesha muwe pamoja siku zote, 16 si mtumwa tena, bali ni zaidi ya mtumwa; kama ndugu mpendwa. Nampenda sana lakini wewe utampenda zaidi, sio tu kama kaka katika familia yenu, bali pia kama mmoja wa walio katika familia ya Bwana.

17 Ikiwa unanitambua mimi kama niliye mwenye imani moja nawe, basi mpokee Onesimo na umkubali kama vile ambavyo ungenikubali. 18 Endapo amekukosea jambo lo lote au unamdai kitu cho chote, unidai mimi badala yake. 19 Mimi Paulo naandika kwa mkono wangu mwenyewe ya kwamba nitakulipa. Tena sina sababu ya kukumbusha kuwa una deni kwangu juu ya maisha yako. 20 Kwa hiyo kaka yangu, kama mfuasi wa Bwana, tafadhali nipe upendeleo[e] katika hili. Ndipo itakuwa faraja kuu kwangu kama kaka yako katika Kristo. 21 Ninapokuandikia barua hii nina ujasiri mkubwa kwamba utakubaliana nami na najua kwamba utafanya zaidi ya haya ninayokuomba.

22 Pamoja na hayo naomba uniandalie chumba cha kufikia, kwa sababu nina matumaini kwamba kwa maombi yenu nitaachiliwa na kuletwa kwenu.

Salamu za Mwisho

23 Epafra mfungwa pamoja nami katika Kristo Yesu anakusalimu. 24 Marko, Aristarko, Dema, na Luka watendakazi pamoja nami nao wanakusalimu.

25 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.

Footnotes

  1. 1:1 Kristo Yesu Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32: Lk 23:2. Tazama pia Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno.
  2. 1:10 niliyemleta Paulo alimzaa Onesimo katika imani ya Yesu Kristo.
  3. 1:11 anafaa Hapa Paulo anachezea maneno katika jina la Onesimo, lenye maana “anayefaa”. Aidha ni jina lilitumika zaidi kwa watumwa maana waliwafaa mabwana zao.
  4. 1:12 Kwa maana ya kawaida, “Ninamrudisha kwako, kitu ambacho kimekuwa kigumu sawa na kuupoteza moyo wangu.” Hii ni kama njia ya kusema kwamba kumtuma Onesimo ilikuwa kwa Paulo kana kwamba anapoteza kitu muhimu sana kwake kinachotoka ndani mwake.
  5. 1:20 tafadhali nipe upendeleo Paulo hapa anachezea maneno tena katika jina la Onesimo, akitumia kitenzi kinachofanana na jina.