Mathayo 22-24
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Simulizi Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Sherehe
(Lk 14:15-24)
22 Yesu aliendelea kuwajibu viongozi wa Kiyahudi kwa mifano zaidi. Akasema, 2 “Ufalme wa Mungu unafanana na jambo lililotokea mfalme alipoandaa sherehe ya harusi kwa ajili ya mwanaye. 3 Aliwaalika baadhi ya watu. Wakati ulipofika mfalme aliwatuma watumwa wake kuwaambia watu waende kwenye sherehe. Lakini walikataa kwenda kwenye sherehe ya mfalme.
4 Ndipo mfalme aliwaita baadhi ya watumishi wengine zaidi na akawaambia namna ya kuwaambia wale aliowaalika: ‘Njooni sasa! Sherehe imeandaliwa. Nimechinja ng'ombe wangu madume na ndama wanono waliolishwa nafaka, na kila kitu kiko tayari kuliwa. Njooni kwenye sherehe ya harusi.’
5 Lakini watu walioalikwa hawakujali yale waliyoambiwa na watumwa wa mfalme. Wengine waliondoka wakaenda kufanya mambo mengine. Mmoja alikwenda shambani na mwingine alikwenda kwenye shughuli zake. 6 Wengine waliwakamata watumwa wa mfalme, wakawapiga na kuwaua. 7 Mfalme alikasirika sana na akatuma jeshi lake kuwaua wale waliowaua watumwa wake. Na jeshi likauchoma moto mji wao.
8 Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Sherehe ya harusi iko tayari. Niliwaalika wale watu lakini hawakustahili. 9 Hivyo nendeni kwenye pembe za mitaa na mwalikeni kila mtu mtakayemwona, waambieni waje kwenye sherehe yangu.’ 10 Hivyo watumwa wake waliingia mitaani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wabaya na wema na kuwaleta kwenye sherehe. Na jumba la sherehe likawa na wageni wengi.
11 Mfalme alipoingia ili kuwasalimu wageni, alimwona mtu ambaye hakuwa amevaa vazi rasmi la harusi. 12 Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki ilikuwaje ukaruhusiwa kuingia humo? Hujavaa vazi nadhifu kwa arusi!’ Lakini mtu yule hakuwa na neno la kusema. 13 Hivyo mfalme akawaambia baadhi ya wale waliokuwa wanawahudumia watu kwa chakula, ‘Mfungeni mtu huyu mikono na miguu yake na mtupeni gizani, ambako watu wanalia na kusaga meno yao kwa maumivu.’
14 Ndiyo, watu wengi wamealikwa, lakini wachache tu ndiyo waliochaguliwa.”
Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego
(Mk 12:13-17; Lk 20:20-26)
15 Kisha Mafarisayo wakaondoka mahali ambapo Yesu alikuwa anafundisha. Wakapanga mpango wa kumfanya aseme kitu ambacho wangekitumia dhidi yake. 16 Wakawatuma kwake baadhi ya wafuasi wao na baadhi ya watu kutoka katika kundi la Maherode. Watu hawa walipofika kwa Yesu wakasema, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mtu mwema na kwamba daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu, bila kujali ni nani anakusikiliza. Huna wasiwasi namna ambavyo wengine wanaweza wakasema. 17 Sasa tuambie, unadhani ni sahihi kulipa kodi kwa Kaisari au la?”
18 Lakini Yesu alijua kuwa watu hawa walikuwa wanamtega. Hivyo akasema, “Enyi wanafiki! Kwa nini mnajaribu kunitega ili niseme jambo lililo kinyume? 19 Nionesheni sarafu inayotumika kulipa kodi.” Wakamwonesha Yesu sarafu iliyotengenezwa kwa fedha. 20 Kisha Yesu akauliza, “Picha iliyo kwenye sarafu hii ni ya nani? Na jina lililo kwenye sarafu hii ni la nani?”
21 Wakajibu, “Ni picha ya Kaisari na ni jina la Kaisari.”
Ndipo Yesu akawajibu, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake na mpeni Mungu vilivyo vyake.”
22 Waliposikia yale Yesu aliyosema, wakashangaa na kuondoka.
Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu
(Mk 12:18-27; Lk 20:27-40)
23 Siku hiyo hiyo baadhi ya Masadukayo walimjia Yesu. (Masadukayo hawaamini kuwepo kwa ufufuo wa wafu.) Masadukayo walimwuliza Yesu swali. 24 Wakasema, “Mwalimu, Musa alituambia kuwa ikiwa mwanaume aliyeoa atakufa na hana watoto, ndugu yake lazima amwoe mkewe ili aweze kuzaa watoto kwa ajili ya nduguye aliyekufa.[a] 25 Walikuwepo ndugu saba miongoni mwetu. Ndugu wa kwanza alioa lakini akafa bila ya kupata watoto. Hivyo ndugu yake akamwoa mkewe. 26 Na ndugu wa pili akafa pia, jambo hili hilo likatokea kwa ndugu wa tatu na ndugu wengine wote. 27 Mwanamke akawa wa mwisho kufa. 28 Lakini wanaume wote saba walikuwa wamemwoa. Sasa watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, mwanamke huyu atakuwa mke wa yupi?”
29 Yesu akajibu, “Mnakosea sana! Hamjui kile ambacho Maandiko yanasema. Na hamjui lolote kuhusu nguvu ya Mungu. 30 Watu watakapofufuliwa kutoka kwa wafu, wanaume hawataoa wake na wanawake hawataozwa kwa wanaume. Kila mtu atakuwa kama malaika walio mbinguni. 31 Someni kile ambacho Mungu alikisema kuhusu watu kufufuliwa kutoka kwa wafu. 32 Mungu alisema, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’(A) Ni Mungu wa walio hai tu, hivyo hakika watu hawa hawakuwa wafu.”
33 Watu waliposikia hili, waliyashangaa mafundisho ya Yesu.
Amri ipi ni ya Muhimu Zaidi?
(Mk 12:28-34; Lk 10:25-28)
34 Mafarisayo waliposikia kuwa Yesu amewafanya Masadukayo waonekane wajinga nao wakaacha kumwuliza maswali. Kwa hiyo Mafarisayo wakafanya mkutano. 35 Ndipo mmoja wao, aliye mtaalamu wa Sheria ya Musa, akamwuliza Yesu swali ili kumjaribu. 36 Akasema, “Mwalimu, amri ipi katika sheria ni ya muhimu zaidi?”
37 Yesu akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na akili yako yote.’(B) 38 Hii ndiyo amri ya kwanza na ya muhimu zaidi. 39 Na amri ya pili ni kama ya kwanza: ‘Mpende jirani yako[b] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’(C) 40 Sheria yote na maandiko ya manabii yamejengwa katika amri hizi mbili.”
Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?
(Mk 12:35-37; Lk 20:41-44)
41 Hivyo Mafarisayo walipokuwa pamoja, Yesu aliwauliza swali. 42 Akasema, “Nini mawazo yenu juu ya Masihi? Je, ni mwana wa nani?” Mafarisayo wakajibu, “Masihi ni Mwana wa Daudi.”
43 Yesu akawaambia, “Sasa ni kwa nini Daudi anamwita ‘Bwana’? Daudi alikuwa anazungumza kwa nguvu ya Roho. Aliposema,
44 ‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
na nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’[c](D)
45 Ikiwa Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Inakuwaje Masihi ni mwana wa Daudi?”
46 Hakuna Farisayo aliyeweza kumjibu Yesu. Na baada ya siku hiyo, hakuna aliyekuwa jasiri kumwuliza maswali zaidi.
Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini
(Mk 12:38-40; Lk 11:37-52; 20:45-47)
23 Kisha Yesu akazungumza na watu pamoja na wafuasi wake, akasema, 2 “Walimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kuwaambia Sheria ya Musa inasema nini. 3 Hivyo mnapaswa kuwatii. Fanyeni kila wanachowaambia. Lakini maisha yao sio mfano mzuri wa kuufuata. Hawatendi wale wanayofundisha. 4 Hutengeneza orodha ndefu ya kanuni na kujaribu kuwalazimisha watu kuzifuata. Lakini sheria hizi ni kama mizigo mizito ambayo watu hawawezi kuibeba, na viongozi hawa hawatazirahisisha kupunguza mzigo kwa watu.
5 Wao wanatenda mambo mema tu ili waonwe na watu wengine. Hufanya visanduku vidogo vya Maandiko[d] wanavyovaa kuwa vikubwa zaidi. Hufanya mashada ya urembo[e] kwenye mavazi yao ya nje kuwa marefu zaidi ili waonwe na watu. 6 Watu hawa wanapenda kukaa sehemu za heshima kwenye sherehe na kwenye viti muhimu zaidi katika masinagogi. 7 Wanapenda kuitwa ‘Mwalimu’ Na kusalimiwa kwa heshima na watu kwenye masoko.
8 Ninyi nyote ni ndugu, dada na kaka kwa sababu mnaye mwalimu mmoja tu. Hivyo msikubali kuitwa ‘Mwalimu’. 9 Nanyi msimwite mtu yeyote duniani ‘Baba’, maana mnaye Baba mmoja tu, naye yuko mbinguni. 10 Msikubali kuitwa ‘Mwalimu’, kwa sababu mnaye Mwalimu mmoja tu, naye ni Masihi. 11 Kila atakayetumika kama mtumishi ndiyo mkuu zaidi kati yenu. 12 Wanaojifanya kuwa bora kuliko wengine watanyenyekezwa kwa lazima. Lakini watu wanaojinyenyekeza wenyewe watafanywa kuwa wakuu.
13 Ole wenu[f] walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnawafungia watu njia ya kuingia katika ufalme wa Mungu, kwa kuwa ninyi wenyewe hamwingii na mnawazuia wale wanaojaribu kuingia. 14 [g]
15 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki. Mnasafiri kuvuka bahari na nchi nyingine ili kumtafuta mtu mmoja atakayefuata njia zenu. Mnapompata mtu huyo, mnamfanya astahili maradufu kwenda Jehanamu kama ninyi mlivyo!
16 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona. Mnasema, ‘Mtu yeyote akiweka kiapo au nadhiri kwa jina la Hekalu, haimaanishi kitu. Lakini yeyote atakayeweka kiapo kwa kutumia dhahabu iliyo Hekaluni lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 17 Ninyi ni wasiyeona mlio wajinga! Hamwoni kuwa Hekalu ni kuu kuliko dhahabu iliyo ndani yake? Hekalu ndilo huifanya dhahabu kuwa takatifu!
18 Na mnasema, ‘Mtu yeyote akitumia madhabahu kuweka nadhiri au kiapo, haina maana yeyote. Lakini kila anayetumia sadaka iliyo kwenye madhabahu na kuapa au kuweka nadhiri, lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 19 Ninyi ni wasiyeona! Hamwoni kuwa madhabahu ni kuu kuliko sadaka yo yote iliyo juu yake? Madhabahu ndiyo inaifanya sadaka kuwa takatifu! 20 Kila anayeitumia madhabahu kuapa au kuweka nadhiri ni dhahiri anatumia madhabahu na kila kitu kilicho juu yake. 21 Na kila anayetumia Hekalu kuapa au kuweka nadhiri kwa hakika analitumia Hekalu na Mungu, anayeishi ndani humo. 22 Kila anayetumia mbingu kuapa au kuweka nadhiri anakitumia kiti cha enzi cha Mungu na yule aketiye juu yake.
23 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya chakula mnachopata,[h] hata mnanaa, binzari na jira.[i] Lakini hamtii mambo ya muhimu katika mafundisho ya sheria; kuishi kwa haki, kuwa wenye huruma, na kuwa waaminifu. Haya ndiyo mambo mnayopaswa kufanya. Na mwendelee pia kufanya mambo hayo mengine. 24 Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona![j] Ninyi ni kama mtu anayemtoa nzi katika kinywa chake na kisha anammeza ngamia!
25 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnaosha vikombe na sahani zenu kwa nje. Lakini ndani yake vimejaa vitu mlivyopata kwa kuwadang'anya wengine na kujifurahisha ninyi wenyewe. 26 Mafarisayo, ninyi ni wasiyeona! Safisheni kwanza vikombe kwa ndani ili viwe safi. Ndipo vikombe hivyo vitakuwa safi hata kwa nje.
27 Ole wenu walimu wa sheria na ninyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Ninyi ni kama makaburi yaliyopakwa rangi nyeupe, lakini ndani yake yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. 28 Ndivyo ilivyo hata kwenu. Watu wanawatazama na kudhani kuwa ninyi ni wenye haki, lakini mmejaa unafiki na uovu ndani yenu.
29 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii, na kuyaheshimu makaburi ya wenye haki waliouawa. 30 Na mnasema, ‘Ikiwa tungeishi nyakati za mababu zetu, tusingewasaidia kuwaua manabii hawa.’ 31 Hivyo mnathibitisha kuwa ninyi ni uzao wa wale waliowaua manabii. 32 Na mtaimalizia dhambi waliyoianza mababu zenu!
33 Enyi nyoka! Ninyi mlio wa uzao wa nyoka wenye sumu kali! Hamtaikwepa adhabu. Mtahukumiwa na kutupwa Jehanamu! 34 Hivyo ninawaambia: Ninawatuma manabii na walimu wenye hekima na wanaojua Maandiko. Lakini mtawaua, mtawatundika baadhi yao kwenye misalaba na kuwapiga wengine katika masinagogi yenu. Mtawafukuza kutoka katika mji mmoja hadi mwingine.
35 Hivyo mtakuwa na hatia kutokana vifo vyote vya watu wema wote waliouawa duniani. Mtakuwa na hatia kwa kumwua mtu wa haki Habili, na mtakuwa na hatia kwa kuuawa kwa Zakaria[k] mwana wa Barakia mliyemwua kati ya Hekalu na madhabahu. Mtakuwa na hatia ya kuwaua watu wote wema walioishi kati ya wakati wa Habili mpaka wakati wa Zakaria. 36 Niaminini ninapowaambia kuwa mambo haya yote yatawapata ninyi watu mnaoishi sasa.
Yesu Awaonya Watu wa Yerusalemu
(Lk 13:34-35)
37 Ee Yerusalemu, Yerusalemu! Unayewaua manabii. Unawapiga kwa mawe wale ambao Mungu amewatuma kwako. Mara nyingi nimetaka kuwasaidia watu wako. Nimetaka kuwakusanya watu wako kama kuku anavyowakusanya vifaranga wake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu kufanya hivyo. 38 Sasa Hekalu lako litaachwa ukiwa kabisa. 39 Ninakwambia, hautaniona tena mpaka wakati utakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’”(E)
Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao
(Mk 13:1-31; Lk 21:5-33)
24 Yesu alipokuwa anaondoka eneo la Hekalu, wanafunzi wake walimwendea na kumwonyesha majengo ya Hekalu. 2 Akawauliza, “Mnayaona majengo haya? Ukweli ni kuwa, yataharibiwa. Kila jiwe litadondoshwa chini, hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jiwe jingine.”
3 Baadaye, Yesu alipokuwa ameketi mahali fulani katika Mlima wa Mizeituni, Wafuasi wake walimwendea faraghani. Wakasema, “Twambie mambo haya yatatokea lini. Na nini kitatokea ili kutuandaa kwa ajili ya ujio wako na mwisho wa nyakati?”
4 Yesu akajibu, “Mjihadhari! Msimruhusu mtu yeyote awadanganye. 5 Watu wengi watakuja na watatumia jina langu. Watasema, ‘Mimi ndiye Masihi.’ Na watawadanganya watu wengi. 6 Mtasikia kuhusu vita vinanavyopiganwa na pia matetesi ya kuwapo vita vingine. Lakini msiogope. Mambo haya lazima yatokee na mwisho wenyewe hautafuata palepale. 7 Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. Utakuwepo wakati wa njaa ambapo watu watakosa chakula. Na kutakuwa matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8 Mambo haya ni mwanzo wa matatizo, kama uchungu wa kwanza mwanamke anapozaa.
9 Kisha mtakamatwa na kupelekwa kwa wenye mamlaka ili mhukumiwe na kuuawa. Watu wote katika ulimwengu watawachukia kwa sababu mnaniamini mimi. 10 Nyakati hizo watu wengi wataacha kuwa wafuasi wangu. Watasalitiana na kuchukiana. 11 Manabii wengi watatokea na kusababisha watu wengi kuamini mambo yasiyo ya kweli. 12 Kutakuwepo na uovu mwingi sana duniani kiasi kwamba upendo wa waaminio wengi utapoa. 13 Lakini yeyote yule atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 14 Na Habari Njema niliyoihubiri kuhusu Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote. Itatawanywa katika kila taifa. Kisha mwisho utakuja.
15 Nabii Danieli alizungumza kuhusu ‘jambo la kutisha litakalosababisha uharibifu.’[l] Mtakapoliona jambo hili la kutisha limesimama patakatifu.” (Asomaye hili anapaswa kuelewa jambo hili linamaanisha nini.) 16 “Watu walio Uyahudi wakimbilie milimani. 17 Wakimbie pasipo kupoteza muda ili kuchukua kitu chochote. Wakiwa darini wasiteremke ili kuchukua kitu na kukitoa nje ya nyumba. 18 Wakiwa shambani wasirudi nyumbani kuchukua koti.
19 Itakuwa hali ngumu kwa wanawake wenye mimba na wenye watoto wachanga! 20 Ombeni isiwe majira ya baridi au isiwe siku ya Sabato mambo haya yatakapotokea na mkalazimika kukimbia, 21 kwa sababu utakuwa wakati wa dhiki kuu. Kutakuwepo na usumbufu mwingi sana kuliko ule uliowahi kutokea tangu mwanzo wa ulimwengu. Na hakuna jambo baya kama hilo litakalotokea tena.
22 Lakini Mungu amekwisha amua kuufupisha wakati huo. Ikiwa usingefupishwa, hakuna ambaye angeendelea kuishi. Lakini Mungu ataufupisha ili kuwasaidia watu aliowachagua.
23 Wakati huo watu wataweza kuwaambia, ‘Tazama, Masihi yuko kule!’ Au wakasema, ‘Ni yule!’ Msiwaamini. 24 Manabii wa uongo na masihi wa uongo watatokea na kufanya miujiza na maajabu[m] makuu, ili ikiwezekana wawadanganye wateule. 25 Na sasa nimewatahadharisha kuhusu hili kabla halijatokea.
Yesu Atakaporudi Tena
(Mk 13:24-31; Lk 17:23-24,37; 21:25-32)
26 Inawezekana mtaambiwa, ‘Masihi yuko jangwani!’ Msiende jangwani kumtafuta. Mtu mwingine anaweza akasema, ‘Masihi yuko katika chumba kile!’ Msiamini. 27 Mwana wa Adamu atakapokuja, kila mtu atamwona. Itakuwa kama radi inavyowaka angani na kuonekana kila mahali. 28 Ni kama kutafuta mzoga: Mzoga hupatikana mahali ambapo tai wengi wamekusanyika.
29 Mara baada ya mateso ya siku hizo, mambo haya yatatokea:
‘Jua litakuwa jeusi,
na mwezi hautatoa mwanga.
Nyota zitaanguka kutoka angani,
na kila kitu kilicho angani
kitatikiswa kutoka mahali pake.’[n]
30 Kisha kutatokea ishara angani kuwa Mwana wa Adamu anakuja. Watu wote wa ulimwengu watajipiga kifuani wakiomboleza. Kila mtu atamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani akiwa na nguvu na utukufu mkuu. 31 Naye atatumia parapanda kuu kuwatuma malaika zake kila mahali duniani. Nao watawakusanya wateule wake kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine.
32 Jifunze kwa mtini: Matawi yake yanapokuwa ya kijani na laini na kuanza kutoa majani mapya, ndipo mnatambua kuwa majira ya joto yamekaribia. 33 Katika namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yakitokea, mtajua kuwa wakati[o] umekaribia wa kile kitakachotokea. 34 Ninawahakikishia kuwa mambo haya yote yatatokea wakati ambao baadhi ya watu wa nyakati hizi wakiwa bado hai. 35 Ulimwengu wote, dunia na anga vitaangamizwa, lakini maneno yangu yatadumu milele.
Mungu Peke Yake Ndiye Ajuaye Siku ya Kurudi kwa Mwana wa Adamu
(Mk 13:32,35; Lk 17:26-30,34-36)
36 Hakuna anayeijua siku wala wakati. Malaika wa mbinguni hawaijui hata Mwana hajui itakuwa lini. Baba peke yake ndiye anayejua.
37 Mwana wa Adamu atakapokuja, itakuwa kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu. 38 Siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuwatoa binti zao kuolewa mpaka siku ambayo Nuhu aliingia kwenye safina. 39 Hawakujua juu ya kilichokuwa kinaendelea mpaka mafuriko yalipowajia na kuwaangamiza wote.
Ndiyo itakavyokuwa Mwana wa Adamu atakapokuja. 40 Wanaume wawili watakuwa wakifanya kazi shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
42 Hivyo iweni tayari daima. Hamjui siku ambayo Bwana wenu atarudi. 43 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua wakati ambao mwizi atakuja? Mnajua angelikesha ili mwizi asivunje na kuingia. 44 Hivyo, ninyi nanyi iweni tayari. Mwana wa Adamu atakuja katika wakati msiomtarajia.
Watumishi Wema na Wabaya
(Mk 13:33-37; Lk 12:41-48)
45 Fikiria mtumishi aliyewekwa na bwana wake kuwapa chakula watumishi wake wengine katika muda uliopangwa. Ni kwa namna gani mtumishi huyo atajionyesha kuwa ni mwangalifu na mwaminifu? 46 Bwana wake atakaporudi na kumkuta anafanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha kwa mtumishi huyo. 47 Ninawaambia bila mashaka yoyote kuwa, bwana wake atamchagua mtumishi huyo awe msimamizi wa kila kitu anachomiliki yule Bwana.
48 Lakini nini kitatokea ikiwa mtumishi huyo ni mbaya na akadhani kuwa bwana wake hatarudi karibuni? 49 Ataanza kuwapiga watumishi wengine na kuanza kunywa na kula na walevi. 50 Ndipo bwana wake atakuja wakati asioutarajia, ambapo mtumishi hakujiandaa. 51 Bwana atamwadhibu mtumishi huyo na kumpeleka anakostahili kuwapo pamoja na watumishi wengine waliojifanya kuwa wema. Huko watalia na kusaga meno kwa maumivu.
Footnotes
- 22:24 nduguye aliyekufa Tazama Kum 25:5,6.
- 22:39 jirani yako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.
- 22:44 chini ya udhibiti wako Kwa maana ya kawaida, “kuweka chini ya miguu”.
- 23:5 visanduku vidogo vya Maandiko Visanduku vidogo vya ngozi vyenye Maandiko manne muhimu. Baadhi ya Wayahudi walivifunga visanduku hivi kwenye vipaji vya nyuso zao na mkono wa kushoto kuonesha kumpenda au uaminifu wao kwa Mungu na Neno lake. Mafarisayo wengi walitengeneza visanduku hivi vikubwa kuliko vya wengine kuonesha kuwa wao ni watu wa dini kuliko watu wengine.
- 23:5 mashada ya urembo Urembo uliotengenezwa kwa nyuzi za sufu au manyoya ya kondoo zinazotambaa mpaka chini kutoka pembe nne za vazi la kusalia au vazi la maombi lililovaliwa na Wayahudi. Urembo huu ulipaswa kuwa ukumbusho wa amri za Mungu (tazama Hes 15:38-41).
- 23:13 Ole wenu Ama Itakuwa vibaya kwenu enyi walimu wa sheria na Mafarisayo.
- 23:14 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 14: “Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo. Ninyi ni wanafiki. Mnawadanganya wajane na kuchukua nyumba zao. Kisha mnafanya maombi marefu ili watu wawaone. Mtapata adhabu mbaya zaidi.” Tazama Mk 12:40; Lk 20:47.
- 23:23 Mnampa Mungu … mnachopata Sheria ya Musa iliwataka Waisraeli kumtolea Mungu sehemu ya kumi ya mazao yao (tazama Law 27:30-32; Kum 26:12).
- 23:23 mnanaa, binzari na jira Haya ni mazao yaliyotolewa malipo ya fungu la kumi. Lakini sheria ya Musa halikujumuisha mazao madogo kama haya yaliyotajwa hapa. Bali Mafarisayo walikuwa wanatoa zaidi ili kuwa na uhakika kuwa hawavunji Sheria.
- 23:24 lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona Hii ina maana kuwa “Mnajishughulisha kwa mambo madogo sana lakini mnatenda dhambi kubwa.”
- 23:35 Habili, Zakaria Katika Agano la Kale la Kiebrania, hawa ni watu wa kwanza na wa mwisho kuuawa. Tazama Mwa 4:8-11 na 2 Nya 24:20-25.
- 24:15 jambo … uharibifu Tazama Dan 9:27; 12:11 (pia Dan 11:31).
- 24:24 miujiza na maajabu Hapa ina maana ya kazi za ajabu zinazofanywa kwa kutumia nguvu za Shetani.
- 24:29 Tazama Isa 13:10; 34:4.
- 24:33 wakati Wakati ambao Yesu aliuzungumzia ni ule ambapo kitu muhimu kitatokea. Tazama Lk 21:31, pale ambapo Yesu anasema huu ni wakati wa Ufalme wa Mungu kutufikia.
© 2017 Bible League International